Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Sayyid Mujtaba Husayni Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuzaliwa Bibi Zainab (s.a.) na Siku ya Wauguzi, ameitaja nafasi ya wanawake na wasichana wa Kizainab wa Iran, katika kipindi cha mwamko wa kipekee wa taifa la Iran kuwa ya kushangaza. Aidha, akirejelea nafasi ya wauguzi katika kufufua matumaini na kuleta uhai, pamoja na athari kubwa waliyonayo katika kulinda afya na usalama wa kimwili na kiroho wa jamii, amewashauri viongozi na maafisa wanaohusika na sekta ya afya kuwapa kipaumbele cha pekee wauguzi.
Ifuatayo ni matini kamili ya ujumbe huo:
Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu.
Tarehe tano ya mwezi wa Jumada al-Ula ya kila mwaka hutukumbusha kuzaliwa mwanamke mtukufu ambaye alikulia chini ya kivuli cha upendo, malezi na kuwa pamoja na watu watano watoharifu (a.s.), ambao Mwenyezi Mungu amrehemu na amsalimu yeye pamoja nao, ambao wanahesabiwa kuwa viumbe bora kabisa katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu.
Malezi na kukua Zainab al-Kubra (s.a.) katika shule hii yenye nuru kwa kipindi cha zaidi ya miaka hamsini kulidhihirisha ndani ya nyota hii angavu ya zama mchanganyiko wa sifa nyingi za heshima na ubora. Sifa hizo zimeendelea kuwa chanzo cha kusifiwa, kupongezwa na kujivunia na mawalii wa Mwenyezi Mungu. Kilele cha mwangaza huo kilidhihirika katika tukio la kishujaa la Ashura, kwa upande mmoja, kulikuwa na huruma isiyo na kikomo, nia njema na kuwajali kwa subira waliodhulumiwa katika jangwa la Karbala; na kwa upande mwingine, alidhihirika kama mojawapo ya vielelezo vya juu kabisa vya uthabiti, uimara na ushujaa.
Tangu mwanzo wake, historia ya harakati na Mapinduzi ya Kiislamu imejaa matukio ya kushiriki wanawake na wasichana wa Iran wenye mwenendo wa Kizainab. Jambo hili lilifikia kiwango cha kushangaza, kwa ubora na wingi, katika kipindi cha mwamko wa kipekee wa taifa, kilichojitokeza wakati wa Vita vya Kujihami Vilivyoanzishwa dhidi ya Iran kwa Mara ya Tatu (Difa-e Muqaddas ya Tatu).
Kwa sasa, wanawake wa Kizainab wa Iran, kupitia ushiriki wao mkubwa katika nyanja mbalimbali, hususan katika viwanja vya mapambano vilivyopo mijini na vijijini, wamekuwa mstari wa mbele katika kufafanua kwa vitendo na kuendeleza muqawama nyuma ya mistari ya vita vya moja kwa moja. Hali imefikia kiwango ambacho watawala madhalimu wa zama hizi, ambao daima wanatamani kuona taifa hili likiteseka, likiumia na kukandamizwa, hawajioni kuwa na uwezo wa kukabiliana na jeshi hili kubwa la wanawake.
Watu wa nchi hii, ambao wamejawa na mapenzi kwa Ahlul-Bayt watoharifu (a.s.), kwa kuzingatia sifa ya huruma, kuelewana na kuwafariji wenye maumivu, pamoja na kujitolea kwa ajili yao, wameamua kwa haki kuifanya siku ya kuzaliwa Zainab al-Kubra kuwa Siku ya Kumuenzi Muuguzi.
Hii ni kwa sababu nyingi ya sifa hizo za kimaadili na thamani za kibinadamu zinaonekana wazi katika kundi hili la wauguzi, ambao ni watu wenye thamani kubwa na wanaofanya kazi kwa juhudi na kujituma.
Nafasi ya muuguzi, kama ilivyo kwa baadhi ya makundi mengine kama vile madaktari, walimu na walezi, wanazuoni wa dini pamoja na wahudumu wa uokoaji na misaada, ni nafasi yenye uwezo wa kufufua matumaini na kuleta uhai. Kwa sababu hiyo, wakati mwingine muuguzi hutazamwa kama malaika wa rehema. Hali hii hutokea pale anapokabiliana na tabia zisizofaa na hali ya kukosa subira ya watu wenye maumivu na wanaoteseka, kisha akawawezesha kupata utulivu, matumaini, nafuu na matibabu, na hatimaye kuwa sababu ya kushuka kwa rehema za Mwenyezi Mungu.
Bila shaka, tofauti na madaktari, nafasi ya wauguzi katika matibabu ya wagonjwa inahitaji uwepo wa muda mrefu, ufuatiliaji wa karibu na wa kuendelea, pamoja na subira. Athari za uwepo wa aina hii huzidi masuala ya kimwili, kwani huwa tiba ya maumivu ya kisaikolojia na kiroho, na katika hali nyingi huzuia kukata tamaa kusitawale ndani ya wagonjwa. Hivyo ndivyo mambo ambayo yako nje ya uwezo wa madaktari pekee yanavyoweza kukamilishwa kupitia utekelezaji wa jukumu hili la kujali na lenye huruma.
Katika zama hizi ambapo mtandao muovu wa ubeberu haufanyi juhudi yoyote ya kuacha bila kutumia aina mbalimbali za dhuluma na uhalifu dhidi ya mataifa huru na yenye msimamo wa muqawama, hususan taifa la Iran, na ambapo miongoni mwa mbinu zake ni kuweka vikwazo vya aina mbalimbali vinavyohusiana na matibabu na dawa kwa lengo la kulilazimisha taifa kubwa la Iran kuvumilia mateso, kuwajali wauguzi, kuimarisha jumuiya ya wauguzi, na kuhifadhi pamoja na kuinua kiwango cha maarifa, ujuzi, uwezo, uchangamfu, ari na heshima yao, hasa wale ambao wamejitoa kikamilifu kufanya kazi katika taasisi zisizo za binafsi, kuna athari kubwa katika kulinda afya na usalama wa kimwili na kiroho wa jamii.
Kwa hiyo, matarajio yangu ni kwamba viongozi na maafisa wanaohusika na sekta ya afya, sambamba na mwenendo wao wa kuwajibika na kujitolea, watayapa masuala haya muhimu kipaumbele kinachostahili.
Ninatoa pongezi zangu kwa taifa langu pendwa, kwa wanawake wa nchi hii ya Kiislamu ambao wanatekeleza majukumu yao kwa dhamira na nia thabiti, na hasa kwa dada na ndugu zangu wauguzi, kwa mnasaba wa maadhimisho haya mawili.
Mwishoni, ninaiomba rehema ya Mwenyezi Mungu kwa mashahidi waliodhulumiwa na waliojitolea kutoka katika jumuiya ya wauguzi, hususan wauguzi mashahidi wa Vita vya Kujihami Vilivyoanzishwa dhidi ya Iran kwa Mara ya Pili na ya Tatu, pamoja na wale waliouawa katika fitna ya mwezi wa Dey mwaka 1404 wa kalenda ya Hijria ya Jua.
Ninatumaini kwamba, kwa dua za bwana wetu, Imam wetu (Mwenyezi Mungu aharakishe kudhihiri kwake), Mwenyezi Mungu Mtukufu atalijalia taifa la Iran heshima na nguvu zaidi kuliko hapo awali, pamoja na kila jambo linalostahili kwa wale wanaofuata shule ya mafundisho ya Zainab (s.a.).
Sayyid Mujtaba Husayni Khamenei
24 Mehr 1405/ Oktoba 16 2026.
Maoni yako